Uhasindisi Kilimo
.
Uboreshaji wa Umechanishaji wa Kilimo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inatekeleza jitihada mbalimbali za kuendeleza utafiti na matumizi ya umechanishaji wa kilimo kwa kubuni, kuboresha na kuhimiza matumizi ya mashine, zana, na vifaa vya kilimo ili kuongeza ufanisi, kupunguza uchovu kwa wakulima, na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, TARI inaendelea kufanya ubunifu na uboreshaji wa mashine mbalimbali za kilimo zinazolenga kupunguza muda wa kazi shambani na kuongeza uzalishaji.
Miongoni mwa mafanikio ya hivi karibuni ni Mashine ya kupanda mbegu ya Rafiki Planter, pamoja na mashine ya kupandia mpunga inayoweka mbolea kwa wakati mmoja. Mashine hizi zimebuniwa ili kuongeza usahihi wa shughuli za kilimo na kupunguza upotevu wa rasilimali.
Utafiti na ubunifu unaofanywa na TARI katika nyanja ya umechanishaji ni sehemu muhimu ya mageuzi ya sekta ya kilimo, yakilenga kuongeza ustahimilivu wa kilimo, tija ya uzalishaji, na kuchangia katika usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi wa taifa.