Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

Tari,Wadau Waadhimisha Siku ya Udongo Duniani.
03 Dec, 2025
Tari,Wadau Waadhimisha Siku ya Udongo Duniani.

 

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na wadau mbalimbli waadhimisha Siku ya Udongo Duniani leo Desemba 3, 2025, Katika Viwanja vya Maonesho ya Nane nane vya Dkt. John Samwel Malecela, Jijini Dodoma. Lengo la maadhimisho hayo ni kutoa hamasa, elimu na msukumo wa kitaifa na kimataifa kuhusu umuhimu wa udongo kama msingi wa maisha na maendeleo ya viumbe hai.

Akifungua maadhimisho hayo Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya kilimo  anayesimamia maendeleo ya mazao na usalama wa chakula Dkt. Stephen J. Nindi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, alisema kuwa udongo ndio chimbuko la shughuli za kiuchumi, ustawi wa jamii na uhai wa ikolojia nzima katika maisha ya binadamu. Ndio maana kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu inasema kuwa “Afya ya Udongo kwa Ustawi wa Miji.” Alisisitiza kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ustawi wa makazi yetu na afya ya udongo na kufafanua kuwa Miji haiwezi kustawi bila chakula, na chakula hakiwezi kuzalishwa bila udongo wenye afya njema. Mgeni Rasmi pia alisema baadhi ya shughuli zinazofanyika zina athari hasi kwa afya ya udongo na katika mabadiliko ya tabianchi. Akibainisha kuwa uharibifu wa udongo unaongezeka kwa kasi nchini Tanzania, Afrika na Duniani kote hali inayosababishwa na matumizi ya ardhi yasiyo endelevu, ukataji wa miti, ufugaji holela, shughuli za kilimo zisizo zingatia utaalamu, ujengaji wa majengo holela na uchimbaji wa madini holela shughuli ambazo zimesababisha upotevu wa takribani asilimia 30 ya rutuba ya udongo kwa miongo miwili yopita.

Mgeni Rasmi aliainisha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uendelevu wa afya ya udongo kwa ustawi wa binamu, chakula na makazi. Wizara ya Kilimo inaendesha zoezi la tathimini ya afya ya udongo katika halmashauri zote, wizara itaendelea kutenga bajeti kwaajili ya afya ya udongo na imegawa vifaa vya upimaji wa udongo katika halmashauri ili kuwezesha wakulima kupima afya ya udongo sambamba na kuwajengea uwezo maafisa ugani nchini kuhusu matumizi ya vifaa hivyo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana alisema Taasisi kupitia maabara zake hufanya tathimini na upimaji ya udongo ili kubaini viwango vya virutubishi kamavile naitrojeni, fosforasi, potasiamu na kaboni. Aidha, Taasisi hufanya vipimo vya tindikali kwaajili ya mapendekezo ya mazao na mbolea kwa matumizi kulingana na aina mahususi ya udongo.

Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Prof. Peter L. Msofe, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya makamu wa Rais na Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Asimwe.