Ofisi ya Waziri Mkuu, TARI zashirikiana kutoa mafunzo ya Kilimo

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, vijana, Ajira na wenye ulemavu (KVAU) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameanza kutoa mafunzo kwa wakulima na waongeza thamani katika mazao mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo uliofanyika Oktoba 21, 2025 Jijini Dodoma, Naibu katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Bi. Zuhura Yunus amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kutoa huduma bora zaidi katika sekta ya kilimo.
Ametaja Mikoa itakayofanyika mafunzo hayo na mazao husika kuwa ni Dodoma zao la Zabibu, Singida zao la Alizeti, Iringa zao la mchicha lishe na nyanya, Mkoa wa Mbeya matumizi ya mitambo midogo ya kilimo, Maharage na parachichi ambapo jumla ya Wakulima elfu moja wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Thomas Bwana ameshukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuitambua TARI na kuipatia jukumu la kuendesha mafunzo hayo suala ambalo ameahidi kulitekeleza kwa ufasaha kupitia wataalamu wake katika maeneo husika.
Wakitoa neno la shukrani kwa nyakati tofauti, wanufaika wa mafunzo hayo wamepongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na TARI kuendesha mafunzo hayo ambayo wanasema yatawasaidia kuongeza tija katika kilimo kwa kukifanya kibiashara.