Manual for crop production according to ecological agricultural zones
  • By CHONA.MAHUSHI
  • Manuals
Publication Year : 2022

Author(s) : Ministry of Agriculture

Kulingana na taarifa za Kituo cha Utafiti wa Udongo cha Mlingano (TARI-Mlingano) Tanzania ina jumla ya Kanda kuu saba (7) za Kiutafiti wa Kilimo na Kanda ndogo 64 za kiikolojia zinazoonyesha aina ya mazao yanayoweza kuzalishwa. Kanda kuu hizo ni Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa. Pamoja na Tanzania kuwa na Kanda Kuu saba (7) za Utafiti wa Kilimo na kanda ndogo 64 za Kiikolojia, kwa muda mrefu tija katika uzalishaji wa mazao hayo imekuwa ndogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mazao kutozingatia kanda hizo za kilimo za kiikolojia. Aidha, gharama za uzalishaji wa mazao nje ya ikolojia yake ni kubwa hususan wakati miundombinu ya umwagiliaji maji inapohitajika. Mwongozo huu utasaidia kufikia azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuwa mazao yatazalishwa kulingana na ikolojia na hivyo kutoa malighafi ya mazao kwa viwanda vinavyojengwa nchini. Uwepo wa viwanda hivyo utaongeza kasi ya uwekezaji katika kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa na kwa gharama nafuu. Mwongozo umeainisha ni wapi na ni zao gani linastahili kuzalishwa. Kwa mfano, maeneo yanayopata mvua chache yatatumika kwa kuzalisha mazao yanayostahimili ukame kama vile Mtama, Muhogo, Viazi vitamu na mazao ya jamii ya mikunde (mbaazi na kunde). Ili mwongozo utumike kikamilifu, pia kalenda ya kilimo imeandaliwa kwa kuzingatia mwenendo wa mvua katika mikoa mbalimbali nchini. Hata hivyo, kwa kuwa kumekuwepo na mabadiliko ya tabianchi kilimo kinachohimili mabadiliko hayo kinahamasishwa, pia wadau katika sekta ya kilimo wanashauriwa kuwasiliana na watafiti na wataalam wa kilimo walioko katika maeneo yao. Serikali itaendelea kuhimiza huduma za ugani zitolewe kwa kuzingatia mwongozo. Mamlaka za Mikoa na Wilaya zinashauriwa kutunga sheria ndogo katika maeneo yao na kubuni njia bora za kutumia mwongozo huu. Wizara itaendelea kutoa maelekezo pale yanapohitajika ili kuhakikisha lengo la mwongozo huu linafikiwa. Mwongozo huu pia unapatikana katika tovuti ya Wizara www.kilimo.go.tz.